WAGOMBEA urais nchini Kenya wanatarajia kuumana katika mdahalo utakaowakutanisha viongozi hao na kuoneshwa moja kwa moja kupitia runinga. Mdahalo huo ambao ni wa kwanza kabisa katika historia ya nchi hiyo na unaotarajiwa kupima uwezo wa wagombea hao juu ya masuala muhimu ya kitaifa unafanyika wakati joto la kampeni likiwa juu hivi sasa.
Mjadala huo ambao unafanyika baada ya juhudi za vyombo vya habari nchini Kenya, unatarajiwa kufuatiliwa na mamilioni ya watu ndani na nje ya mipaka ya Kenya kupitia njia za mitandao ya kijamii pamoja na magazeti, huku vituo vinane vya televisheni, vituo 34 vya redio vikitegemewa kuutangaza moja kwa moja tukio hilo.
Kwa awamu hii ya kwanza, mdahalo huo utajikita kuangalia masuala ya uongozi, huduma za kijamii, afya na elimu pamoja na usimamizi wa rasilimali bila ya kuliacha nyuma suala la usalama.
Wagombea sita wa urais – Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Musalia Mudavadi, Martha Karua, Peter Kenneth na James Ole Kiyiapi – watapambana kujibu masuali na kujieleza juu ya walivyojiandaa kuyatatua matatitizo ya Wakenya katika ajenda zitakazojadiliwa.
Watangazaji watakaohusika kuwabana wagombea hao kujibu masuali yaliyoandaliwa na jopo maalum la waandalizi wa mdahalo huo ni Linus Kaikai kutoka kituo cha televisheni cha Nation na Julie Gichuru akiwa ni mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Citizen jijini Nairobi. Mdahalo huo utakaoanza saa 1:30 magharibi kwa saa za Afrika Mashariki utafanyika katika ukumbi wa shule ya kimataifa ya Brookehouse jijini humo.
Bunge la mwanzo baada ya uchaguzi wa 2007 nchini Kenya. Mdahalo huo unafanyika katika wakati ambapo tafiti za maoni zilizofanywa na mashirika mbalimbali zikionesha kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 4 Machi yatakuwa ni ya kukaribiana kabisa, hasa kati ya wagombea wakuu wawili – Raila Odinga kutoka muungano wa CORD na Uhuru Kenyatta akishikilia bendera ya muungano wa Jubilee – huku ikitajwa kuweko uwezekano mkubwa wa kufanyika duru ya pili.
Kwa mujibu wa mashirika ya kukusanya maoni ya Ipsos Synovate na Infotrack wapiga kura ambao watafuatilia kwa makini zaidi mdahalo huo ni wale ambao hadi sasa hawajaamua ni nani anayestahili kupigiwa kura kuliongoza taifa hilo kubwa kiuchumi katika eneo la Afrika Mashariki.
Wadadisi wa mambo wanasema mdahalo huo wa kwanza kabisa kuwahi kufanyika nchi humo unaweza kuwa chachu muhimu kwa wapiga kura juu ya mtu wa kumpigia kura, ingawa mtazamo utakaojitokeza baada ya mdahalo juu ya vipi matokeo ya uchaguzi yanavyoweza kuwa ni suala litakalotegemea mambo mengi.
Lakini, juu ya hilo, wakati zikiwa zimesalia wiki tatu tu kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu na kukitarajiwa mdahalo wa pili tarehe 25 Februari, ni wazi mdahalo huo unaweza kabisa kuwashawishi wapiga kura wengi kujitokeza kuitafuta hatma ya nchi yao.
No comments:
Post a Comment