MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal ameongoza waumini wa Kiislamu kuupokea mwaka mpya wa Kiislamu katika hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya Istikaama (ISTIQAAMA) tawi la Dar es salaam.
Sherehe hizo za kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu 1434 Hijriyya ambazo zilifanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam zilihudhuriwa na waumini wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali pamoja na mabalozi wa Sudan, Oman na Iran nchini Tanzania.
Akizungumza na waumini hao Dk. Bilal aliwataka Waislamu kuuanza mwaka mpya wa Kiislamu kwa kuepuka machafuko na kudumisha amani ambao ndio msingi mkuu wa dini ya Kiislamu.
Makamu wa Rais alisema katika serikali wameanza kuingia wasi wasi kutokana na vurugu za hivi karibuni ambazo zimeashiria kuvunjika kwa amani nchini.
“Mimi na wenzangu Serikalini tumeanza kuingia wasi wasi. Hivi karibuni katika nchi yetu kumetokea vurugu ambazo hatimaye zimeashiria kuvunjika kwa amani ya nchi yetu. Mali zimepotea na wengine wamepoteza maisha kwa kisingizio cha dini,” alisema Dk. Bilal na kuongeza
“Machafuko hayo yametufanya tujiulize hawa watu wanafuata misingi ipi ya Dini ambayo imewafanya wao wawe na jazba kiasi cha kushindwa kuwa na busara katika maamuzi yao. Je ni vipimo vipi vya msingi wa Dini ambavyo wao wanavifuata. Tunashindwa kupata jawabu”.
Makamu wa Rais aliwaeleza waumini hao kuwa kwa mawazo yake anaona matatizo mengi yanayolenga Uislam ni ukosefu wa elimu, ile ya Uislam wenyewe, na elimu ya dunia na kuwataka Waislamu kusoma kwa dhati jambo ambalo anaamini linaweza kusaidia mambo ya jazba yakapungua na hatimaye kutokomea kabisa.
“Tukiendeleza jazba ndio ziwe na nguvu kuliko mafunzo ya Quran tukadhani kuwa mwenye jazba ndiye Muislamu wa kweli tutaharibikiwa,” alibainisha. Akisoma risala ya Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Nassor Alhinai aliiomba serikali kuifanya siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiislamu kuwa ni ya mapumziko
Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, AlhajiMussa Salum alikubaliana na wazo hilo lakini aliwataka Waislamu wenyewe kubadilika kwa kuitangaza tarehe hiyo ya kwanza ya mwaka mpya kwa kuipa nafasi katika maisha yao ya Kiislamu ili iweze kutambulika ipasavyo.
No comments:
Post a Comment