Sunday, February 10, 2013

AZAM YAFANYA KWELI KWA MTIBWA

AZAM FC imeikamata Yanga SC kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja Manungu, Turiani, Morogoro jioni hii.
Ushindi huo unaifanya Azam ifikishe pointi 33 sawa na Yanga SC, ingawa Wana Lamba Lamba wamecheza mechi moja zaidi.
Yanga inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, kwani imefunga mabao 29, imefungwa 12 na Azam sasa imefunga mabao 27, imefungwa 14.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Azam ilitangulia kupata bao dakika ya 14, lililofungwa na beki wake Mkenya, Joackins Atudo, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Wakata Miwa..
Mtibwa, mabingwa wa Ligi Kuu mara mbili 1999 na 2000, walisawazisha bao hilo dakika ya 21, mfungaji winga wa zamani wa Yanga, Vincent Barnabas, aliyeuwahi mpira baada ya kipa wa Azam, Mwadini Ali kuteleza wakati amerudishiwa mpira na beki wake, Atudo.
Hadi mapumziko, timu hizo ziliwa zimefungana bao 1-1 na kipindi cha pili Azam walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata mabao ya ushindi.
Azam ilipata bao lake la pili dakika moja tu tangu kuanza kipindi cha pili, 46, lililotiwa kimiani na mshambuliaji Mganda, Brian Umony aliyepokea pasi ya kiungo Mkenya, Humphrey Mieno.
Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche alifunga mabao mawili ndani ya dakika mbili za mwisho na kuunenepesha ushindi wa Azam.
Alifunga bao la tatu dakika ya 89, akimalizia pasi nzuri ya Mieno na la nne alifunga baada ya kupokea pasi nzuri sana ya Salum Abubakar 'Sure Boy.'
Yanga itashuka dimbani Jumatano kumenyana na vibonde, African Lyon ili kufikisha idadi ya mechi sawa na Azam na Simba SC zinazofukuzana katika mbio za ubingwa.
Simba SC waliotoa sare ya 1-1 na JKT Oljoro jana mjini Arusha, wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 28.

No comments:

Post a Comment