TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
1. Kamati ya Ligi jana (Oktoba 29,2012) ilifanya kikao
pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kujadili mambo kadhaa,
likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia televisheni na radio kutangaza
moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni
kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati ilifanya mazungumzo
na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto
kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala yafuatayo:
a- kwamba uamuzi wa
kuzuia vituo vya redio na televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi
lakini una kasoro katika utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa
vyombo vya habari na pia haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari
kufanya maandalizi kwa kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.
b- Kwamba Kamati ya Ligi haijakataza redio kutangaza moja
kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya redio ambavyo vinataka kutangaza
moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye hivyo bila ya kuweka matangazo ya
wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa moja yatadhaminiwa, basi vituo
hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.
c- Kwamba vituo vya redio vitakavyotaka kutangaza moja kwa
moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke mashindano hayo kuwa ni “Ligi Kuu
ya Vodacom”.
d- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kutangaza moja
kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni lazima viingie mkataba na TFF ambao
utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa, kituo cha televisheni cha Star TV
hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo hiyo hadi hapo
mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba huo utasainiwa kabla ya mechi za
kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali kuendelea
kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.
e- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kuchukua picha
kwa ajili ya habari zinaruhusiwa kufanya hivyo. Endapo kituo hicho kitaonesha
mchezo uliorekodiwa, hatua zitachukuliwa dhidi ya kituo hicho.
f- Kamati inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na
uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa lengo zuri
la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoziwezesha klabu kujimudu
kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom iendeshwe kwa ubora zaidi.
2. Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim Poulsen
amerejea Dar es salaam baada ya kufanya ziara kwenye visiwa vya Pemba na Unguja
ambako alishuhudia mechi sita za Ligi Kuu ya Grand Malta kuanzia Oktoba 19,
2012 hadi Oktoba 26, 2012 visiwani Zanzibar. Poulsen alishuhudia mechi baina ya
Falcom na Bandari iliyoisha kwa Falcom kushinda kwa mabao 3-1 na pia mechi
baina ya Duma na Bandari ambayo iliisha kwa Bandari kuibuka na ushindi wa mabao
2-0. Mechi hizo mbili zilifanyika kisiwani Pemba .
Poulsen pia alishuhudia mechi zilizofanyika kwenye Uwanja wa
Amaan kisiwani Unguja ambako Mtendeni iliibwaga Chipukizi kwa mabao 2-1; Mundu
na Jamhuri (0-1), KMKM na Zimani Moto (1-0); na Mafunzo dhidi ya Chuoni
iliyoisha kwa Mafunzo kulala kwa mabao 3-0.
Poulsen amefurahishwa na ziara hiyo na kusema kuwa ni kitu
kizuri kwake na kwa soka la Tanzania
kwa ujumla. Poulsen alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyopata visiwani Zanzibar na kukishukuru Chama cha Mpira wa Miguu cha
Zanzibar (ZFA) kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wote akiwa Zanzibar .
Hata hivyo, Poulsen alisema hawezi kueleza kwa sasa kama ameona wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha
Taifa Stars, lakini akasema amevutiwa na viwango vya wachezaji wengi.
3. TFF inapenda tena kuihimiza klabu ya Yanga kumalizana na
mchezaji wake wa zamani, John Njoroge Mwangi kabla ya Novemba 2, 2012 ili
ijiepushe na adhabu kaili inayoweza kuchukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la
Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa barua ya FIFA, iwapo Yanga
haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na kusiwepo na mawasiliano yoyote, shauri hilo litawasilishwa
kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba 14, 2012 kutathmini
hukumu iliyotolewa mapema Januari mwaka huu.
4. Mchezo namba 10 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baina ya
Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto mjini Tabora Oktoba 31, 2012,
sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni ambayo Morani walikuwa
wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati wakitoka Kigoma ambako
walicheza na Kanembo.
5. TFF inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa zilizotolewa na
baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo gazeti la Habari Leo na Daily News,
vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga akisema kuwa amewataka watu wanaotaka
kugombea uongozi wa shirikisho watangaze nia ili wapate kujadiliwa. Waandishi
walioandika habari hiyo hawakumnukuu vizuri Rais Tenga wakati akizungumzia
masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha maana nzima ambayo Ndg. Tenga alitaka
iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira wa miguu. Rais Tenga alivitaka vyombo
vya habari vianzishe mjadala utakaowashirikisha wapenzi wa mpira wa miguu ili
waelezee wanatarajia nini katika miaka ijayo na hivyo kuwafanya viongozi
watakaochaguliwa kufanya kazi kwa utashi wa maoni hayo ya wananchi. Tunaelewa
kuwa Rais Tenga ni muumini wa kuheshimu katiba, sheria na kanuni na hivyo
hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka mchakato wa uchaguzi wa TFF kwa kuwataka
wanaowania uongozi kutangaza nia sasa badala ya kusubiri muda wa kikanuni ufike.
Ikumbukwe katika kikao chake na wahariri aliwahi kuulizwa swali kama hilo na akasema kuwa
akijibu lolote atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kuwa itamaanisha anaanza
kampeniu kabla ya muda. Ni vizuri waliohusika wakafanya masahihisho ili kuzuia
habari zao kutafsiriwa tofauti na wadau wa mpira wa miguu na hivyo kuweka
uwezekano wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
6. TFF imebadilisha tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa watu
wanaotaka kugombea uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es salaam (DRFA) kwa lengo la kuhakikisha
kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa kanuni. Kamati ya Uchaguzi
ya DRFA ilitangaza jana kuwa uchukuaji fomu ungeanza leo, lakini DRFA
iliandikiwa barua jana kuelezwa kuwa mchakato huo sasa utaanza kesho na uchaguzi
utafanyika Desemba 12, 2012.
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA utakuwa kama ifuatavyo:
30/10/2012 Kamati ya
Uchaguzi DRFA kutangaza uchaguzi na nafasi
Zinazogombewa kwa
mujibu wa katiba ya DRFA
31/10/2012 Kuanza
kuchukua fomu za kugombea uongozi
04/11/2012 Mwisho wa
kurudisha fomu ifikapo saa 10:00 alasiri
05-09/11/2012 Kamati
ya Uchaguzi DRFA kupitia fomu za waombaji uongozi na
kutangaza matokeo na
kubandika kwenye mbao majina ya waombaji uongozi.
10-14/11/2012 Kutoa
fursa ya pingamizi dhidi ya waombaji uongozi. Pingamizi
ziwasilishwe kwa
katibu wa Kamati ya Uchaguzi DRFA na
wawekaji pingamizi
wazingatie Ibara ya 11 (2) ya Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama
wa TFF.
15-17/11/2012
Kujadili pingamizi, usaili na kutangaza matokeo ya usaili na
kuwajulisha kwa
maandishi.
18-20/11/2012 Kukataa
rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA
21-25/11/2012 Rufaa kusikilizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
na kutangaza
matokeo ya rufaa (Kama hakuna rufaa, Kamati ya Uchaguzi ya
DRFA kutangaza majina
ya wagombea na nafasi wanazogombea
na kuanza kampeni).
26/11/2012 Baada ya
maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA
kutangaza majina ya wagombea na nafasi zao
na kuanza kwa kampeni
12/12/2012 Uchaguzi
No comments:
Post a Comment